Mweyekiti wa mtsaafu wa kijiji cha Kasenga kata ya Kasenga Bw. Damiani Mlengela emechangia Mbuzi, Jogoo na Gunia la Mahindi kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa kituo cha Afya cha kata hiyo.
Mwenyekiti huyo alitoa mchango huo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel aliyefika kijijini hapo kushirikiana na wananchi kuchimba msingi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha kata hiyo.
“Tangu nizaliwe sijawahi kupata fursa kama hii ya kuchangia shughuli za maendeleo… hivi vitu hata mimi nikifa watoto wangu watachangia ili mradi jengo likamilike” alisema kwa msisistizo Bwana Damiani
Michango mingine iliyopatikana kwenye zoezi lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa ni pamoja na mifuko ya saruji 172, Fedha Taslimu shilingi 130,000, Vyakula na mafuta ya kupikia.
Mkuu wa Mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel amewataka wananchi hao kujitoa ili kujenga kituo cha Afya cha kata hiyo ili badae kisaidie jamii ya eneo hilo. ”Mkiwa na kituo cha afya hapa Kasenga hata mauaji ya kishirikina yatakwisha, mauaji ya kishirikina yanatokana na imani potofu hasa pale kunapokuwa hakuna kituo cha afya cha kuweza kutibu wananchi ” alisema Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Geita amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kutoa mikopo ya mfuko wa wanawake na vijana bila kubagua mahali vikundi hivyo vilipo. Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya Halmashauri kutoa mikopo kwa vikundi vilivyopo mijini na kuviacha vikundi vilivyopo vijijini.
Diwani wa Kata ya Kasenga mhe. Damian Zilahiye amempongeza Mkuuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel kwa kazi ya kuhamasisha na kushiriki na wananchi kujenga vituo vya afya na Zahanati. Amemshukuru pia kwa kuweza kufika na kuwafariji pamoja na kutoa msaada wa fedha taslimu shilingi milioni moja wakati kata hiyo ilipokumbwa na mvua kali zilizombatana na upepo mapema mwezi huu na kusababisha familia kadhaa za kata hiyo kukosa mahali pa kuishi.
Wilaya ya Chato ina jumla ya vijiji 115 mpaka sasa kuna Hospitali moja, zahanati 24 na vituo vya afya 3 vinavyofanya kazi. Majengo mbalimbali ya zahanati na vituo vya afya 68 yapo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.