Halmashauri ya Wilaya ya Chato ni miongoni mwa Wilaya zilizoshiriki kikamilifu maonesho ya nane nane 2025 ambayo katika kanda ya ziwa Magharibi yanafanyika viwanja vya Nyamhongolo Jijini Mwanza huku yakizidi kupamba moto katika banda la wilaya hiyo kutokana na wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu, kununua bidhaa na kupokea ushauri wa kitaalamu kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi kutoka kwa wataalamu waliobobea.
Akizungumza katika maonesho hayo Afisa kilimo, Mifugo na uvuvi (W) Ndg Geriad Mgoba amesema kuwa bidhaa / Huduma zinazopatikana katika banda la Halmashauri hiyo ni elimu kwa vitendo kuhusu kilimo chenye tija, Teknolojia ya uvuvi endelevu ikiwa ni pamoja na uvuvi wa samaki kwa njia ya bwawa, elimu ya ufugaji wa kisasa na upatikanaji wa ndege mbalimbali wakiwemo kuku, njiwa, bata, kuchi na batamzinga, pia elimu ya kuzalisha/kutengeneza malisho bora ya mifugo ili wasitembee umbali mrefu kufuata chakula lakini pia mbwa wenye mafunzo wanapatikana banda la Chato.
Ndg. Mgoba ameongeza kuwa bidhaa nyingine zinazopatikana ni pamoja na asali mbichi za nyuki wadogo na nyuki wakubwa, Mafuta ya alizeti, dagaa waliokaangwa na waliokaushwa kwa jua, Samaki waliokaangwa na waliokaushwa kwa moshi, mashudu, alizeti bila kusahau mboga mboga kama vile vitunguu, Chainizi, biringanya, viazi lishe pamoja na mchicha mwekundu (beetroot) ambao wengi hutumia kwa kuongeza damu mwilini.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu; " Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi 2025" kitaifa yameanza mnamo Agosti 1, 2025 na Kanda ya ziwa Magharibi yalifunguliwa rasmi 03, 8, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela na yatahitimishwa rasmi mnamo Agosti 8, 2025 huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mhe. Said Mtanda Mkuu wa mkoa wa Mwanza.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.