Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chato limepitisha makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi yenye jumla ya shilingi 55,213,189,051 kwa mwaka 2018/2019.
Akiwasilisha bajeti hiyo ya mapato na matumizi mweka hazina wa Halmashauri Bw. Nicholaus Haraba amesema bajeti hiyo inatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri yenye thamani ya shilingi 2,454,191,000, ruzuku ya matumizi ya kawaida shilingi 3,532,262,000, ruzuku ya mishahara shilingi 35,621,075,775, ruzuku ya miradi ya maendeleo shilingi 12,605,660,276 na nguvu za wananchi shilingi 1,000,000,000.
Kupitia bajeti hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Chato inatarajia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019 yenye thamani ya shilingi 16,229,832,544.
Akiwasilisha mpango na bajeti ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Chato afisa mipango wa Halmashauri Bw. Said Abdalah amesema bajeti ya miradi ya maendeleo inatokana na fedha za ruzuku kutoka serikali kuu shilingi 14,177,552,544, mapato ya ndani (60%) shilingi 1,052,280,000 na michango ya jamii kiasi cha shilingi 1,000,000,000. Bw. Abdalah amesema kupitia bajeti hiyo wadau wa maendeleo wanatarajia kuchangia kiasi cha shilingi 142,510,000 katika bajeti hiyo.
Wakichangia bajeti hiyo waheshimiwa madiwani mbalimbali wameshauri bajeti hiyo ilenge zaidi katika kumalizia miradi mbalimbali iliyopo kwenye kila kata na wameomba Halmashauri iongeze bajeti ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Chato.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya YA Chato Mhe. Bartholomeo Manunga amesema utekelezaji wa bajeti hiyo kwa kiasi kikubwa unategemea makusanyo ya mapato ya ndani hivyo amewataka wakuu wa idara pamoja na waheshimwa madiwani kusimamia vizuri suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Shaaban Ntarambe kupitia hotuba yake iliyosomwa na katibu tawala wilaya ya Chato bw. Elias Makory amewataka madiwani kuzingatia vipaumbele muhimu katika bajeti hiyo ili kuleta maendeleo.
Mkuu wa Wilaya amelipongeza baraza la madiwani na Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani (60%) kwa ajili ya akina mama na vijana na amewataka madiwani hao kusimamia vizuri fedha mbalimbali zinazopelekwa kwenye kata.
Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Chato ilipitisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi yenye jumla ya shilingi 58,955,111,068.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.