Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita Oktoba 16, 2025 ilizindua rasmi zoezi la Utambuzi, Usajili, Ufuatiliaji wa Ng'ombe kwa kutumia heleni za Kielektroniki sambamba na utoaji wa Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa iliyoambatana na elimu dhidi ya Magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu hususani kichaa cha Mbwa.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Ofisi ya kata ya Muungano wilayani humo kwa ushirikiano wa timu ya wataalamu kutoka kituo Cha Mifugo kanda ya Ziwa, wataalamu wa Mifugo wa Kata zote za wilaya hiyo wakiongozwa na Daktari wa wanyama wa Wilaya hiyo Dkt Sosthenes J. Nkombe. Daktari Nkombe alisema Halmashauri ya Chato ilipokea dozi za chanjo ya kichaa cha mbwa 1,000, heleni za utambuzi wa ng'ombe 110,000 wakati lengo ni kuchanja mbwa na Paka 6,420 ambapo alieleza kuwa chanjo nyingine zitanunuliwa na Halmashauri hiyo ikiwa nia kubwa ni kulinda afya ya mifugo na wafugaji, kuisajili itambulike sambamba na kuipandisha thamani kwa kuitambua ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa itakayofanyika kwa muda wa miezi miwili kuanzia sasa.
"Chanjo hii ya kudhibiti ugonjwa dhidi ya Kichaa cha Mbwa ni muhimu kwa kulinda afya ya mbwa na mfugaji mwenyewe, pia utambuzi wa Ng'ombe kwa heleni za Kielektroniki na usajili utarahisisha kupata takwimu sahihi zitakazosaidia ufuatiliaji wa mifugo na mazao yake pamoja na mikakati ya kuihudumia, hivyo wafugaji wote mhakikishe mnatekeleza kikamilifu zoezi hili ambalo baada ya uzinduzi huu kila kata itafikiwa" Alisema Dkt Nkombe.
Kwa upande wake Jonas Nyanda mkazi wa kata ya Muungano aliishukuru Serikali kwa kuleta chanjo ya kichaa cha mbwa kwani yeye ni mhanga wa kung'atwa na mbwa, amekiri kuwa alitumia gharama kubwa kupata matibabu hivyo alisema chanjo hiyo itaisaidia jamii nzima kuwa salama.Pamoja na zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo, timu ya wataalamu ilifika Shule ya Sekondari ya Ufundi Chato kutoa elimu dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa wanafunzi kidato cha i - vi ambapo pamoja na elimu nyingine walizopewa juu ya kichaa cha Mbwa pia walifahamishwa huduma ya kwanza baada ya kupata jeraha ni kuliosha na maji
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.