Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Chato ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii (W) Ndg. Elimkwasi John, ilifanya ziara ya siku mbili kukagua Miradi ya ujenzi wa Majosho inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali vilivyopo ndani ya Wilaya hiyo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF).
Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia Agosti 25 - 26, 2025 ilitembelea na kukagua ujenzi wa majosho 15 yanayojengwa katika vijiji vya Kisesa, Kachwamba, Bukome, Nyangomango, Katende, Mkungo, Nyantimba, Kalebezo, Nyabugera, Bwina na Kibehe, Muranda, Ilemela, Bwera, pamoja na Makurugusi huku gharama za miradi hiyo ikiwa ni Tshs. 428,571,430.50
Ndg. Mkwasi alisema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha kuwa ujenzi wa miradi hiyo unazingatia ubora wa viwango vya kitaalamu, unakamilika kwa wakati na unaendana na matarajio ya halmashauri ya kuboresha huduma za mifugo na ustawi wa jamii ambapo timu hiyo ilifurahishwa na hatua za utekelezaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Sosthenes J.Nkombe ambaye ni Daktari wa wanyama (W) alisema uwepo wa Majosho hayo utasaidia kupunguza Magonjwa yanayoenezwa na Kupe na Inzi ambayo mpaka sasa ndiyo yanayosababisha vifo vingi vya ndama, Lakini yanaleta hasara kubwa kwa wafugaji kwa sababu kutibu Ng'ombe aliyeshambuliwa na Magonjwa yanayoenezwa na Kupe ni gharama kubwa.
Aliongeza kuwa kuogesha Ng'ombe kwa kutumia bomba la mkono halina ufanisi ikilinganishwa na kuogesha kwenye Josho, hivyo majosho haya yatapunguza vifo na kuondoa gharama za matibabu kwa wafugaji na kupelekea wafugaji wafuge kwa tija kwa kujipatia kipato na Chakula cha uhakika kwa kipindi chote Cha ufugaji.
Halmashauri ya Wilaya ya Chato itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhakikisha inakamilika kwa ubora unaotakiwa ili kufanikisha lengo kuimarisha uchumi wa kaya na kuongeza tija katika sekta ya mifugo.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.