Kampeni ya kitaifa ya chanjo ya mapafu na utambuzi wa mifugo ilizinduliwa rasmi Septemba 10, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katikati ya mwezi June 2025 akiwa mkoani Simiyu.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Louis Peter Bura katika kijiji cha Nyangomango kata ya Ilemela wilayani humo ambapo amewataka wafugaji kuhakikisha mifugo yao yote inapata chanjo sambamba na kuwekwa heleni ikiwa ni mikakati ya kudhibiti magonjwa ya milipuko kwa mifugo pamoja na kurahisisha utambuzi.
" Chanjo hii ni ruzuku ya Serikali tofauti na chanjo zilizopita, kila ng'ombe atachanjwa kwa Tsh. 500/=, mbuzi Tsh. 300/= lakini kuku ni bure, sasa sisi wafugaji tunatabia ya kuficha ng'ombe wetu ili isijulikane una ng'ombe wangapi, tutoke kwenye dhana hiyo, tunahitaji takwimu kwa faida ya nchi na si vinginevyo, lengo ni kupata mifugo yenye afya bora ili kupata soko zuri ndani na nje ya nchi" Alisema Mhe. Bura
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Mandia Kihiyo pamoja na Kuishukuru Serikali, amekiri kupokea kiasi cha Tsh. 20,940,000/= kwa ajili ya zoezi hilo, chanjo dozi 120,000 kwa ajili ya kuchanja ngombe, chanjo ya kuku dozi 360,000, pikipiki 8, majokofu pamoja na toolbox huku akisisitiza kuwa atawasimamia kwa ukaribu wataalamu wa chanjo na utambuzi mifugo kutekeleza kampeni hiyo kwa wafugaji wote.
Naye daktari wa wanyama wa halmashauri hiyo ambaye ndiye mratibu wa kampeni ya Chanjo Wilayani humo Dkt. Sosthenes J. Nkombe alisema zoezi hilo linakwenda sanjali na utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa kutumia heleni za kielektroniki, hivyo ng'ombe ambao watachanjwa watatambuliwa na baada ya kutambuliwa watasajiliwa na watakuwa wanafuatiliwa ili mfugaji aweze kurasimisha mifugo yake ifahamike na kuondoa changamoto za watumiaji wengine wa ardhi na kupunguza wizi wa mifugo lakini pia kujua kiwango cha huduma kwa mifugo hiyo.
Nkombe aliongeza kuwa halmashauri inakadiria kuchanja Ng'ombe zaidi ya laki 1, wameshachanja 36,193 na kuku 326,751 wamechanjwa
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.