Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Mtemi Msafiri Semeon (kulia) akikabidhi ufunguo wa pikipiki kwa mratibu elimu kata ya Bwanga Venance Bahati
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Eliurd Mwaiteleke akiongea na wakuu wa shule, walimu wakuu na waratibu elimu kata za Chato
Mkuu wa Wilaya ya Chato (katikati) akiwasha pikipiki kama ishara ya kukabidhi pikipiki hizo kwa waratibu wa elimu kata 23 za Wilaya ya Chato
Watendaji mbalimbali wa idara ya elimu wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chato (hayupo pichani)
Serikali Wilayani Chato imeziagiza shule zote kuanzia msimu ujao kuhakikisha zinalima zao la Pamba na Mtama kuanzia ekari mbili kwa kila shule.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Mtemi Msafiri Semeon wakati akiongea na walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu wa elimu kata za Chato kwenye hafla fupi ya ugawaji wa pikipiki 23 zilizotolewa na serikali kupitia wizara ya elimu, sayansi, na ufundi stadi hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
“Tunahitaji shule na taasisi zote ni lazima muwe na ekari zisizopungua mbili za pamba na zinatakiwa kusimamiwa na wagani waliopo huko vijijini” amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya amesema fedha zitakazopatinaka kutokana na zao la pamba ziwe na lengo la kumnufaisha mwanafunzi kwa kuwaandalia chakula ili kumpunguzia mzigo mzazi ambao wamekuwa wakichangia huduma ya Chakula kwa wanafunzi.
Akikabidhi pikipiki hizo Mkuu wa Wilaya amewataka waratibu wa elimu kata kuzitembelea shule zilizopo maeneo yao mara kwa mara na si kusubiri wakati wa mitihani tu kwani sasa wamepata usafiri.
Mkuu wa Wilaya pia amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji kutenga bajeti kwa ajili ya kununua pikipiki za watendaji wa kata kwa awamu ili nao waweze kutimiza malengo yao sambamba na kuwafikia wananchi kilahisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Eliurd Mwaiteleke amesema Wilaya ya Chato imekuwa ikifanya vizuri kwenye matokeo ya elimu hivyo uwepo wa pikipiki hizo kutasaidia katika kuboresha upatikanaji wa elimu ili kuongeza tija na ufaulu ambapo shule zote zitafikiwa kirahisi.
Amewaasa waratibu elimu kata kuzitumia vizuri pikipiki hizo kwa kufanyia kazi za kuboresha elimu na si kufanyia shughuli zao binafsi na kuepuka kuendesha wakiwa wamelewa.
Naye mratibu wa elimu kata ya Bukombe Mwalimu Ernestina Athanas amesema amefurahishwa na ujio wa pikipiki hizo ambapo kwa sasa atazifikia shule 7 za kata hiyo na amesema anategemea matokeo mazuri kwa matokeo yajayo.
Jumla ya pikipiki 23 zimekabidhiwa kwa waratibu wa elimu wa kata za Wilaya ya Chato ambao kuna jumla ya shule za msingi 139 na shule za sekondari 28.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.