Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Mhandisi Deusdedith Katwale amewataka wafanyabiashara wote wanaouza sukari kwa bei ya tofauti na bei iliyoelekezwa na Serikali pamoja na wanaoficha sukari wachukuliwe hatua endapo wataendelea kukaidi agizo kwani wanaowaumiza ni wananchi.
Mhandisi Katwale aliyasema hayo katika kikao maalum cha kamati ya ushauri wilaya kilichofanyika Januari 24/2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Chato ambapo mwenyekiti wa kikao ni Mhe. Mkuu wa wilaya na wajumbe ni Katibu tawala wilaya, Kamati ya ulinzi na usalama wilaya, Mhe. Mbunge, Mhe.Mwenyekiti wa Halmashauri, Maafisa Tarafa wote, Wakuu wa Idara na vitengo,Watendaji kata wote, Viongozi wa vyama vya siasa vyote pamoja na Viongozi wa Mashirika yasiyo ya Serikali.
Aidha Mhandisi Katwale amemtaka mkurugenzi kuwatuma maafisa biashara wa Halmashauri kuwatembelea na kuwapa elimu juu ya ununuzi na uuzaji wa bidhaa hususani sukari kwa kufuata bei zilizoelekezwa na Serikali huku wakiangalia kuhudumia jamii bila kuiumiza na wao kuridhika na faida ndogo wanayoipata.
Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara wilaya ya Chato Ndg Jovin Mugisha Mwarabu alikiri kuwepo kwa changamoto ya sukari hivyo aliiomba Serikali kufanya mazungumzo na wazalishaji wa Sukari kuhusu kupunguza bei ili kuwasaidia wafanyabiashara mbali na kuihudumia jamii lakini pia nao waweze kupata faida tofauti na hivyo watakuwa wanatoa huduma kwa kuinufaisha jamii huku wao wakiingia hasara.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chato Ndg Philip Shoni alisema ameyapokea maelekezo yote ya Mhe. Mkuu wa wilaya na kuahidi kuyafanyia kazi kwa uharaka na kuhakikisha Afisa biashara wa Halmashauri wanawafikia wafanyabiashara ili kuwapa elimu lakini pia kuwasihi wafuate maelekezo ya Serikali.
Akihitimisha kikao hicho kilichoketi kwa lengo la kufanya mapitio ya kujadili utekelezaji wa mpango na bajeti wa mwaka 2024/2025 pia kupokea , kupitia na kushauri vipaombele vya kuingizwa kwenye mpango na bajeti 2024/2025 vitakavyowasilishwa na Halmashauri ngazi ya mkoa.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.