Kamati ya siasa ya mkoa wa Geita imepongeza uamuzi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuamua kujenga hospitali ya rufaa ya kanda iliyopo Chato na wameshauri jitihada mbalimbali za kuitangaza hospitali hiyo zifanyike ili wananchi waweze kuifahamu na kwenda kupata huduma za matibabu hospitalini hapo.
Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Januari 2022 na wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Geita ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Mhe. Said Kalidushi na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM wilayani hapa.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Mhe. Said Kalidushi amesema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika hospitali hiyo ni muda muafaka sasa wa wananchi uifahamu na kufika hospitalini hapo ili kuweza kupatiwa huduma mbalimbali za matibabu badala ya kwenda nje ya nchi ambapo hospitali hiyo hivi sasa imeanza kutoa matibabu kwa wagojwa wa nje.
"Hebu tuitangaze hospitali hii wananchi wote wajue ikoje, hospitali kwa sasa ipo vizuri sana si lazima sana uende hospitali zingine wakati hapa kuna huduma nzuri tena ambazo zamani tulizifuata nje ya nchi" alisema mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amesema kazi nzuri inayofanywa katika katika hospitali hiyo ni kutokana na serikali kutoa fedha kwa wakati ambapo pia amewapongeza wakala wa majengo Tanzania (TBA) kwa kusimamia vyema ujenzi huo.
Wakikagua kikundi cha bodaboda kikichopo Mpogoloni mjini Chato Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita ndugu Said Kalidushi amesema vijana wengi wamekuwa wakipewa mikopo lakini wamekuwa hawajiwekei malengo kutokana na wengi wao kukata tamaa na kudharau kazi ndogo ndogo wanazofanya hivyo amewaasa vijana hao kufanya kazi kwa kujiwekea malengo ili waweze kufikia ndoto zao.
"Nataka niwaambie hizi biashara mnazofanya jiwekeeni malengo ya baadae maana umri unaenda, tumieni vikao mjadiliane namna ya kuboresha maisha yenu ili mfanye mambo makubwa zaidi, mnaweza fikiria kukopa gari badala ya hizi bodaboda mlizo nazo hivi sasa" alisisisitiza mwenyekiti wa CCM mkoa.
Awali wakikagua miradi ya ujenzi wa madarasa yaliyojengwa kutokana mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uviko 19 katika shule shikizi ya Mkombozi na Sekondari ya Buhingo Chato kamati hiyo imeipongeza uongozi wa Wilaya ya Chato kwa usimamizi mzuri na imeagiza kukamilisha kasoro ndogondogo zilizopo ili wanafunzi watakapofungua shule madarasa hayo yaweze kutumika.
Miradi mingine ambayo imekaguliwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya lami Ntarambe km 2 iliyopo Muungano ambayo imegharimu shilingi 1,007,132,000.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.