Serikali ya Japan kupitia ubalozi wa Japan nchini Tanzania imekabidhi ghala la kuhifadhia samaki kwenye soko la samaki la kimataifa la Kasenda lililojengwa kwa ufadhili wa serikali ya Japan.
Soko hilo lililopo kata ya Muganza lina jumla ya wafanyabiashara wa samaki zaidi ya 240 limegharimu jumla cha Shilingi milioni 320 za kitanzania hadi kukamilika kwake ukarabati uliohusisha pia ukarabati wa soko la zamani.
Akikabidhi soko hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Balozi wa Japan nchini Tanzania mhe. Masaharu Yoshida amesema kukamilika kwa ujenzi wa ghala la kuhifadhia samaki na dagaa kutasaidia kuokoa mazao mengi kutoka ziwani hususan samaki na dagaa.
“Soko la samaki la Kasenda halikuwa na miundombinu ya kuhifadhia samaki ambapo zaidi ya tani 200 za samaki zilitupwa kila mwaka kutokana na kuharibika ambapo serikali” alisema Mhe Masaharu.
Wakati huo huo serikali ya Japan imesaini mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Chato ya ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa moja kutoka Muganza hadi Kasenda mahali lilipo soko hilo kwa thamani ya shilingi milioni 197.
Waziri wa Nishati mhe.Dkt. Medard Kalemani ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Chato ameishukuru serikali ya Japan kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania. Amesema serikali ya Japan kwa muda sasa imekuwa ikishirikiana na Wilaya ya Chato na hii imeokana na uhusiano mzuri ulioanzishwa na mbunge wa Chato kwa wakati huo mhe. John Pombe Magufuli.
Mkuu wa Mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel ameishukuru serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na mkoa wa Geita na amewataka wananchi pamoja na uongozi wa soko kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ili kuhakikisha malengo ya uanzishwaji wa soko hilo yanatimia likiwemo suala zima la ukusanyaji wa mapato.
Mbali na kuhudumia soko la ndani ya nchi, soko hilo la kimataifa la Kasenda limekuwa likihudumia baadhi ya nchi za jirani kama vile Congo DCR, Rwanda, Burundi na Uganda. Soko hilo linakadiriwa kukusanya Zaidi ya shilingi milioni 140 kwa mwaka.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.