Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chato leo imekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) ambapo wamepongeza jitihada za Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kusogeza huduma za maji karibu na wananchi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe Martha Mkupasi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maji Wilayani Chato ambapo amesema miradi mingi ya maji imeweza kutekelezwa kwa kipindi cha muda mfupi hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya maji iliyopo katika maeneo yao ili kuepuka uharibifu wa miundombinu hiyo "Tunamshukuru sana mheshimiwa Rais Samia kwa fedha nyingi kwenye miradi ya maji, kazi yetu hapani ni kuendelea kuilinda miundombinu hii ili maji yaendelee kutokana muda wote" amesema Mkuu wa Wilaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato ndugu Mandia Kihiyo amesema hapo awali kulikuwa na tatizo kubwa la uapatikanaji wa maji katika kata ya Kachwamba hususani kwenye kituo cha afya cha Kachwamba ambapo amesema kupitia mradi wa maji wa Imalabupina Ichwankima tayari maji yamefika kata ya Kachwamba hivyo ameshauri RUWASA kuhakikisha huduma ya maji inafika katika taasisi zote zilizopo wilayani hapa.
Mkurugenzi Mtendaji pia amesema mwezi Oktoba na Novemba 2022 katika kata ya Kachwamba pekee, serikali ya awamu ya sita imeleta fedha kiasi cha shilingi milioni 400 za kujenga shule mpya msingi Ipandikilo na shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Sekondari Buhingo-Chato.
Diwani wa kata ya Ilemela Mhe. fortunatus Jangole emesema kukamilika kwa mradi wa maji wa Nyambogo Ilemela ni jambo la faraja kubwa kwa wananchi hao, hivyo amewataka wananchi wa kata ya Ilemela kuitunza vyema miundonbinu hiyo.
Diwani wa kata ya Kachwamba mhe. Stela Masabile amesema kupatikana maji katika kata hiyo kutasaidia kupunguza adha kubwa ya maji ambayo imekuwa ni tatizo sugu na la muda mrefu kwa wananchi hao.
Naye diwani wa kata ya Muganza mhe. Emmanuel Nyamuranga amesema kukamilika kwa miradi wa maji wa Muganza kutapunguza tatizo la maji kwa wananchi wapatao elfu 30 wa kata hiyo hivyo amemshukuru mhe Rais kwa kuweza kuwakumbuka wananchi wa Muganza.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Chato mhandisi Avitus Exavery amesema kwa sasa miradi ya maji ya Nyambogo Ilemela, na Kachwamba imeshakamilika na imeanza kutoa huduma ambapo mradi wa Muganza Bwongera unaendelea kutekelezwa ambapo umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika mnamo tarehe 30 Januari 2023.
Miradi iliyotembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ni pamoja na mradi wa maji wa Nyambongo Ilemela, Kachwamba na Muganza Bwongera
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.