Mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bi. Fransisca Charles aliongoza kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa kampeni ya mazingira pamoja na kuwapitisha wajumbe wa kikao kwenye takwimu za usafi wa mazingira ambapo kilihusisha maafisa afya wote waliopo katika Halmashauri hiyo.
Kikao hicho kilifanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Septemba 15 hadi 16, 2025 katika ukumbi mdogo wa mikutano uliopo jengo la Uthibiti Ubora wa Shule lililopo karibu na jengo la Halmashauri hiyo ambapo kila Afisa afya aliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yake.
Bi. Fransisca aliwataka maafisa afya hao kuzingatia usafi wa mazingira unaotengeneza soko (MBS) ikihusisha upatikanaji wa huduma kwa wote hususani katika suala la vifaa vya ujenzi wa vyoo bora vijijini, kutokana na mbinu hiyo kusaidia jamii kupanda kiwango cha usafi pamoja na kupunguza jamii kurudi nyuma hata baada ya majanga ya mafuriko.
"Maafisa afya wenzangu nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya hususani kazi kubwa mliyoifanya wakati wa maandalizi ya ujio wa Mwenge wa Uhuru 2025 wilayani kwetu, nawakumbusha pia kuendelea kuifanyia kazi kikamilifu kauli mbiu yetu isemayo" Mtu ni afya" ambayo inajipambanua katika maeneo ya ujenzi bora wa vyoo, unawaji mikono, hedhi salama, usafishaji wa mazingira, lishe, udhibiti taka pamoja na ufanyaji wa mazoezi, pia tuzingatie kutumia Community Led Total Sanitation (CLTS) wakati wa ukaguzi wetu kwenye kaya maana kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaitendea haki taaluma yetu na tutapata mazingira safi lakini pia tunatengeneza jamii yenye afya bora." Alisema Bi Fransisca
Pamoja na kujadili hali ya utekelezaji wa majukumu pia kikao hicho kiliweka maazimio ambayo kila mmoja alitakiwa kwenda kuyatekeleza kwa ufasaha ambayo ni ukaguzi wa chumvi zinazouzwa madukani na Sokoni kuzia kuuzwa chumvi zisizo na madini joto, kudhibiti uuzaji holela wa vyakula, kufuatilia uwepo wa vyoo bora kwenye Ofisi za taasisi hususani shule na vituo vya kutolea huduma za afya ili ziwe mfano wa kuigwa na jamii, kuzingatia uhakiki wa takwimu za kaya wanazohudumia, kukusanya mapato ya kitengo husika na halmashauri kwa ujumla.
Halmashauri ya wilaya ya Chato ina jumla ya Kaya 70,697 kutoka kata 23 na vijiji 115, ambazo zinahudumiwa na maafisa afya 06 na 02 kutoka makao makuu ya wilaya hiyo wanaohakikisha jamii inakuwa katika hali ya usafi na kupata afya njema ili waweze kuendelea kutekeleza majukumu yao pamoja na ya Serikali kikamilifu.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.