Maonesho ya teknolojia ya madini kimataifa yamefunguliwa rasmi leo Septemba 23, 2023, Mkoani Geita na Mhe. Doto Biteko ambae ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya EPZ bomba mbili, Mjini Geita, Dkt. Biteko ameiagiza Benki Kuu kuweka mkakati wa kununua dhahabu kwa bei ya soko na wachimbaji wadogo wafikiwe kokote waliko kupewa elimu.
Aidha, ameeleza kuwa, sekta ya madini imechangia kwa kiasi kikubwa kuchagiza uchumi wa Taifa, hasa katika mkoa wa Geita. Hivyo basi wadau wa sekta hiyo watumie fursa zilizopo kujiongezea kipato cha mtu mmojammoja na jamii kwa ujumla.
“Tuna kila aina ya utajiri unaoonekana kwa macho na usioonekana kwa macho ambao lazima tuutafsiri kuwaondolea shida na umaskini watu wetu. Mhe. Rais anatamani kupitia sisi wasaidizi wake tubadilishe rasilimali hizi kuwa utajiri” Amesema Mhe. Biteko
“Naomba nimshukuru sana Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya madini, mageuzi ambayo yanashudiwa leo yamekuja kwa sababu ya uongozi Madhubuti wa Raisi wetu” Ameongeza Dkt. Biteko
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, amesema mkoa umewezesha kugawa leseni 1118 kwa wachimbaji wadogo katika mkoa wa kimadini Mbogwe na leseni 1231 mkoa wa kimadini Geita.
Wadau mbalimbali wa sekta ya madini wamejitokeza kushiriki maonesho hayo muhimu, bila kusahau Halmashauri za Mkoa wa Geita zimeshiriki katika maonesho hayo makubwa kila mwaka.
Maonesho ya teknolojia ya madini mwaka 2023 yanabebwa na kauli mbiu isemayo “Matumizi ya Teknolojia Sahihi Katika Kuinua Wachimbaji Wadogo Kiuchumi na Kuhifadhi Mazingira”
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.