Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa wilaya Chato kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chato.
Akiongea na washiriki wa Mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Chato Eng. Deusdedith Katwale akizindua mafunzo hayo amewataka watumishi wote wa umma kuongeza ubunifu wa kuwahudumia wananchi kwa ubora wa hali ya juu badala ya kufanya kazi kwa mazoea.
Mbali na uwajibikaji wametakiwa kujenga uhusiano mzuri wa kiutumishi,kwa kuheshimiana kupendana,kuthaminiana na kusaidiana kwa kuwa wote lengo lao kubwa ni kuwahudumia wananchi ili wapate maendeleo yanayokusudiwa na serikali.
Mhe. Deusdedith Katwale Katwale,ameyasema hayo mapema hii leo 26 Mei 2023 ambapo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wa pamoja wa namna bora ya kuwatumikia wananchi tunaowaongoza.
"Mafunzo haya natarajia yatatujengea uelewa wa pamoja katika kuwaongoza wananchi tunaowatumikia, aidha leo tumeifanya kuwa siku ya mapumziko kwa kuwa kila binadamu anahitaji muda wa kupumzika...na pia itusaidie kujenga mahusiano mazuri na ushirikiano wa umoja wetu kwa kuwa watumishi wote ni familia moja inayolenga kumhudumia mwananchi"
Akitoa mafunzo hayo kwa Watumishi wa Umma wilaya ya Chato, Mtaalamu wa Mafunzo ya Huduma kwa Wateja ngazi ya Kiwango cha Kimataifa, Ndg. James Mwang'amba amesema miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatia kwa watumishi wa umma ni kufanya kazi kwa ubora zaidi ya wengine.
Hata hivyo amedai malalamiko mengi ya wananchi hutokana na baadhi ya watumishi wa umma kufanya kazi chini ya ubora unaotakiwa, huku akitoa mfano kwa baadhi ya watumishi ambao huingia kazini pasipo kujali muda wa kazi, kutoroka kazini na wengine kutokuwa na lugha rafiki kwa wananchi wanaohitaji huduma.
Kadhalika amewataka kuwa na mikakati yenye ubunifu wa kuwatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kuutumia muda wao wa mapumziko vizuri ikiwemo kulala mapema na kujiepusha na misongo ya mawazo jambo linaloweza kushusha ufanisi wao wa kazi.
Katika hatua nyingine Mwang'amba amewataka watumishi wa umma kubadilika kifikra ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuboresha utendaji wao wa kazi jambo litakalo wavutia wananchi kupata huduma wanazotarajia badala ya kuendelea kulalamika kila uchao.
Kwa upande wake,Ofisa ugani kata ya Chato,Evelline Kamzola,amepongeza uwepo wa mafunzo hayo na kwamba yamewasaidia kuwakumbusha namna ya kutimiza majukumu yao wakati wakiwahudumia wananchi ikiwemo kutumia lugha rafiki kwa wateja wao.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri ya wilaya ya Chato,kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, maofisa tarafa,watendaji wa kata,waratibu elimu kata,watendaji wa vijiji,na baadhi ya watumishi wengine waliojitokeza.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.