Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta ameonya tabia ya baadhi ya watu wanaotoa kauli za uchochezi unaolenga kudhohofisha uhusiano wa kirafiki, kidugu na kijirani uliopo kati ya Kenya na Tanzania na amebainisha kuwa vitendo hivyo haviwezi kuruhusiwa kuwagawa Wakenya na Watanzania.
Mhe. Rais Kenyatta amesema leo wakati akiwasalimu wananchi muda mfupi baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Chato Mkoani Geita katika siku ya kwanza ya ziara yake binafsi ya kumtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyepo mapumzikoni Chato Mkoani Geita.
Amefafanua kuwa Tanzania na Kenya zimejaaliwa kuwa na mali nyingi, kuongea lugha moja ya Kiswahili na wananchi wake wanashirikiana kwa mambo mengi, hivyo kauli ama vitendo vyovyote vinavyolenga kuharibu uhusiano huu mzuri havikubaliki na havitafanikiwa.
“Nimekuja hapa Chato kama ndugu, jirani na rafiki. Na hii ndio Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sisi tunataka, sio jumuiya ya watu ambao wana fikira ndogo, za zamani, za kikabila, za ujinga, sisi tunataka jumuiya ya watu wenye maono ya mbele, ambao wanajua kwamba Kenya ikitajirika Tanzania imetajirika, Tanzania ikitajirika Kenya imetajirika, watu ambao hawawagawi watu kwa mambo madogomadogo ambayo hayasaidii” amesema Mhe. Rais Kenyatta.
Mhe. Rais Kenyatta ameongeza kuwa katika uongozi wake anatamani kuona Jumuiya ya Afrika Mashariki inaungana na kuwa kitu kimoja, wananchi wake wanakuwa huru kwenda nchi yoyote ndani ya jumuiya na ametoa wito kwa wana Afrika Mashariki kujielekeza katika kuzijenga nchi zao kimaendeleo badala ya kupoteza muda mwingi kwa porojo za kisiasa.
Amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazizofanya kujenga uchumi wa Watanzania na pia amepongeza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato ambao amesema utasaidia kukuza biashara, ujenzi wa viwanda na uwekezaji mwingine katika eneo hilo na nchi jirani.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Kenyatta kwa kuomba kuja kumtembelea akiwa mapumzikoni Chato, na amebainisha kuwa ziara yake ni uthibitisho kuwa uhusiano wa Tanzania na Kenya ni mzuri na Wakenya na Watanzania ni wamoja.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa uhusiano wa Tanzania na Kenya umeanza kabla ya uhuru ambapo Watanzania wanaona Kenya ni nyumbani kwao na Wakenya wanaona Tanzania ni nyumbani kwao, na kwamba nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mengi ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Kenyatta kwa kukemea na kuchukua hatua dhidi ya kiongozi mmoja wa siasa nchini Kenya aliyetoa kauli za kichochezi zilizolenga kuharibu uhusiano mzuri wa Watanzania na Wakenya na amemhakikishia kuwa Watanzania wanawapenda Wakenya.
Amesisitiza kuwa Tanzania na Kenya zinashirikiana katika miradi mingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Arusha – Namanga – Arthi River nchini Kenya, vituo vya huduma za pamoja vya mipaka ya Holili na Namanga, na hivi sasa mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili – Taveta, mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Kenya na maandalizi yanaendelea ya kujenga barabara ya lami ya Bagamoyo (Tanzania) – Mombasa (Kenya).
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.