Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amezindua rasmi ushirika wa wavuvi wa mwalo wa Kikumbaitale uliopo kata ya Kigongo wilayani hapa.
Akizindua ushirika huo Mhe. Ulega amewaasa wana ushirika hao kuimarisha ushirika huo ili uwe na tija katika kuendeleza shughuli zao na hatimaye kuboresha maisha yao ya kila siku.
Katika uzinduzi hu, ushirika huo ulipewa fedha kiasi cha shilingi milioni tano kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuendeleza uvuvi salama ziwani ambapo pia Naibu Waziri Ulega ameziasa taasisi zingine za fedha kuvisaidia vyama hivyo vya ushirika kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ili wavuvi waweze kufanya shughuli za uvuvi kwa kutumia zana salama.
Aidha Naibu Waziri amemwagiza mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuhakisha wanaanza ukarabati wa bwawa la Katende lililopo kata ya Katende ambalo limeharibika kwa kiasi kikubwa na kusababisha wananchi wengi hususan wafugaji wa kata ya Katende na maeneo ya jirani kupata usumbufu wa maji kwa mifugo yao.
Amesema kwa kuanzia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itatoa shilingi milioni 10 za ukarabati wa bwawa hilo ili liweze kuhudumia wafugaji kwa haraka zaidi.
Waziri wa Nishati na Mbunge wa jimbo la Chato Mhe. Medard Kalemani ambaye alikuwepo kwenye ziara hiyo ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuuwezesha ushirika huo wa wavuvi wa mwalo wa Kikumbaitale na kuwataka wanaushirika hao kutumia vyema raslimali zitakazonunuliwa kutokana na fedha hizo. Aidha Mhe. Kalemani ameshukuru pia Wizara hiyo kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ukarabati wa Bwawa hilo ambalo ni tegemeo kwa wakazi wa Katende.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.