Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita, itaungana na maeneo mengine hapa Nchini kuanza mtihani wa upimaji wa Kitaifa kwa darasa la nne, unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 22 hadi 23 ikiwa na Jumla ya wanafunzi 18,604 waliosajiliwa kufanya mtihani huo ambapo kati yao Wavulana ni 8798 na Wasichana 9806.
Afisa Elimu (W) idara ya msingi Mwl John Bassu amesema Halmashauri hiyo ina jumla ya shule 166 kati ya hizo 154 ni shule za Serikali na 12 ni za Binafsi.Mwl Basu ameeleza kuwa walimu wametimiza majukumu yao kikamilifu kwa kuwafundisha watahiniwa na kumaliza mada mapema ikiwa ni pamoja na kuwapa mazoezi ya kutosha ili kuwajengea umahiri utakao wasaidia kujibu mtihani wao vizuri.
Mkurugenzi Mtendaji (W) Ndg Mandia Kihiyo amekiri kuwa maandalizi ya Mtihani yamekamilika kwa kuwapatia mafunzo na maelekezo ya kina wasimamizi wote wa mitihani lengo likiwa ni kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufanisi unaotarajiwa."Walimu wote watakaosimamia mtihani wamepewa semina elekezi na wameandaliwa vizuri kwa kufuata mwongozo wa Baraza la Mitihani pamoja na vyombo husika vinavyounda kamati ya mitihani, ulinzi na usalama upo imara kuhakikisha kazi inafanyika kwa usalama wa hali ya juu bila udanganyifu" Alisema Kihiyo.Aidha Ndg Kihiyo amewatakia Mtihani mwema wanafunzi wote wa Darasa la Nne 2025.Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania ilitoa ratiba ya mtihani wa Darasa la Nne mwaka 2025 kuwa unatarajia kuanza Oktoba 22 na kuhitimishwa Oktoba 23, 2025.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.