Bibi Sigwa Bushuwandama mkazi wa kijiji cha Mkungo kata ya Bukome kupitia mpango wa TASAF 3 ameanzisha ufugaji wa Mbuzi na Kondoo kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato cha familia yake yenye watoto watano
Bwana Mapinduzi Elkana (kulia) baada ya kuanza kunufaika na mpango wa TASAF 3 aliamua kuchimba kisima na kuanza kuuza maji kwa wakazi wa kijiji cha Mkungo ambapo kwa siku anakadiria kuuza ndoo 40 sawa na shilingi 4000 kwa siku
Bibi Tekla Mashine mkazi wa kijiji cha Kanyama kata ya Ilemela baada ya kuanza kunufaika na mpango wa TASAF 3 alianza kufuga mbuzi mradi ambao umemwezesha kuweka umeme wa jua kwenye nyumba yake na kupeleka watoto 6 shule ya msingi na sekondari
Bibi Nyamarwa Justine mkazi wa kijiji cha Kanyama kata ya Ilemela Wilayani Chato mbali na ufugaji wa mbuzi ameweza kujenga nyumba ya vyumba vitatu na matarajio yake ni kukamilisha ujenzi huo mwaka 2019.
Bi Maria Jacob mkazi wa kijiji cha Nyang’omango kupitia mpango wa TASAF 3 ameweza kununua vyombo vyua kisasa kwa ajili ya matumizi ya familia yake.
Baadhi ya wanufaika wa mpango wa TASAF awamu ya tatu Wilayani wameendelea kujiongezea kipato kwa kufuga aina mbalimbali za mifugo.
Baadhi ya wanufaika wamesema kupitia ufugaji wameona ndio njia pekee ya kwao kujikwamua na hali ngumu ya maisha ambayo walikuwa nayo kabla ya kuingia kwenye mpango wa TASAF 3 wa kunusuru kaya masikini.
Bi Sugwa Bushuwandama mkazi wa kijiji cha Mkungo kata ya Bukome Wilayani hapa anasema kupitia mpango wa TASAF 3 kwa kipato kidogo anachopata hivi sasa anao mbuzi 12 ambao mara kwa mara amekuwa anauza na kununua mahitaji mengine ya familia kama vile chakula.
“mwezi uliopita niliuza mbuzi wawili nilienda kufanya manunuzi mnadani ambapo nilinunua gunia la mahindi la shilingi elfu 40 na nguo za wanangu” alisema Bi Sugwa huku akitabasamu.
Kwa upande mwingine wanufaika hao wanasema kupitia miradi ya ufugaji wa Ng’ombe na mbuzi kwao imekuwa ni rahisi kutokana na urahisi pindi wanapotaka kuuza au kubadili kupata bidhaa nyingine kama vile chakula pindi familia zinapokuwa kwenye ukata.
Bi Lega Amos mkazi wa kijiji cha Nyambiti kata ya Nyamirembe ambaye ana mbuzi 17 amesema baada ya kuanza kunufaika na mpango wa TASAF 3 alianza kununua mbuzi wawili lakini hadi sasa kupitia ufugaji huo ameanzisha mradi wa kukaanga samaki na kuuza kwenye soko la kijijini hapo lakini pia ameweza kujenga nyumba ndogo ya tofali za tope na kuezeka kwa bati.
“sasa hivi naweza kulisha, kuvalisha na hata kusomesha hawa watoto ambao wote ninawalea, Nina nyumba ya bati lakini pia ninaishi vizuri na familia yangu” alisema Bi Lega.
Kwa ujumla wanufaika wengi wa mpango wa TASAF 3 Wilayani Chato wamejikita zaidi kwenye ufugaji wa Mbuzi na Ng’ombe ambao kwao wanasema huleta matokeo ya haraka wakati familia ikiwa kwenye wakati mgumu wa kiuchumi.
Kupitia miradi hiyo ya ufugaji wanufaika hao wameomba kutembelewa na wataalamu wa mifugo kwa ajili ya ushauri wa ufugaji bora pamoja na utengenezaji wa mabanda imara kwa ajili ya mifugo yao.
Wilaya ya Chato ina jumla ya wanufaika wa TASAF awamu ya tatu 7,666 Kati yao wanufaika 1000 Wamejikita kwenye miradi ya ufugaji wa mbuzi na Ng’ombe na baadhi wameanzisha biashara ndogo ndogo kama njia ya kujiongezea kipato cha kaya.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.