Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi leo machi 25, 2024 imetoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani wa mifugo ngazi ya Vijiji na Kata wa
mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera (Kanda ya ziwa Magharibi) lengo likiwa ni kuendelea kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu pamoja na kutatua changamoto za wafugaji waliopo maeneo yao ya kazi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni katibu Tawala wa Wilaya Mhe. Thomas Dime amewataka maafisa mifugo kutumia mafunzo waliyopata kuwaelimisha wafugaji namna ya kufuga kisasa, Lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao yake ili kuleta mabadiliko kiuchumi katika jamii.
Naye Afisa Tawala Mkuu kutoka wizara ya mifugo na uvuvi Bw. John Kusaja amewasihi maafisa mifugo kujitathmini katika utendaji kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi na kufuata, haki na wajibu wa mtumishi ili kupata matokeo mazuri kiutendaji hususani katika sekta ya Mifugo.
" Mtumishi wa umma unatakiwa kufanya kazi kwa kuhakikisha unafuata taratibu, sheria na kanuni kwa kuzisoma na kuzielewa ili kutambua haki zako hata unapozifuatilia ujue unachostahili na taratibu za kupata, wajibu ni kile ambacho mtu analazimika juu ya jambo fulani na haki ni jambo au kitu ambacho mtu anapaswa apate na lazima itimizwe ikiwa haijatimizwa inadaiwa" Alisema Kusaja
Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa na timu ya wataalam kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Kanda ya ziwa Magharibi kuanzia machi 25, 2024 na kuhitimishwa Machi 26, 2024 huku mada mbalimbali zikiwasilishwa ili kuwaimarisha maafisa mifugo katika kuongeza na kujikumbusha utaalamu wao katika kutekeleza majukumu yao wakiwa kazini.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.