Mkuu wa Wilaya ya Chato Mh. Louis Bura leo Oktoba 6,2025 amefungua rasmi Zahanati ya Kijiji cha Kanyindo iliyopo Kata ya Nyarutembo,Tarafa ya Bwanga, Wilayani Chato. Zahanati hii inategemea kuhudumia takribani wananchi 5,085 wa Kijiji cha Kanyindo na vijiji jirani.
Akiongea na wananchi wakati wa ufunguzi,Mh.Bura amewapongeza wanakijiji wa Kanyindo kwa kuonesha mfano bora kwa kushirikiana na wawekezaji ili kujiletea maendeleo na Mkurugenzi na timu ya Mganga Mkuu kuhakikisha wanasimamia Zahanati kukamilika na kuanza kutoa huduma. “ Hii ni Wilaya yangu ya 4 kuongoza,ila wewe ni Mkurugenzi mwenye kasi ya utendaji wa kuleta maendeleo!Unasimamia maelekezo ya serikali vizuri na kukusanya mapato ipasavyo”
Mh. Bura ameomba viongozi na wananchi kuendelea kufanyia kazi mapungufu madogo ili huduma itolewe kwa Ubora na Mwakani Zahanati hii izinduliwe na Mwenge wa Uhuru! “ La muhimu sana niwaombe ndugu zangu wa Kanyindo,mshirikiane vizuri na watumishi,msigombane nao baada ya kuanza huduma mahali hapa!Pia watumishi tumieni uwezo wenu wote kutoa huduma bora kwa watanzania kulingana na mazingira yaliyopo” Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Ndg. Mandia Kihiyo amewapongeza wananchi wa kijiji cha Kanyindo kwa kubuni mradi mkubwa wa zahanati na kujitoa kwa nguvu zao zote kujenga zahanati hadi kukamilika! “Kama halmashauri tunawapongeza na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha huduma bora zinapatikana hapa zahanati na tumeongeza fedha taslimu million 3 kwaajili ya ujenzi wa kichomea taka ili huduma za kujifungua kwa kina mama zianze haraka”.Akishukuru kwa niaba ya Wananchi wa kijiji cha Kanyindo Bi Sidonia Paulo ameushukuru uongozi wa Wilaya kwa kuhakikisha wanapata huduma ya afya baada ya kusubiri kwa miaka 8 “tunashukuru sana zahanati hii kufunguliwa na tutaanza kupata huduma karibu kwani awali tulikua tunasafiri umbali wa zaidi ya kilomita 7 kwenda kujifungua Nyarutembo”.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.