Mganga mkuu Dr Daniel Mzee, ameongoza kikao cha maandalizi ya Ufunguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyarututu kilichopo Kata ya Bwanga. Akiongoza kikao hicho Dr Mzee amewapongeza uongozi wa Kijiji,wajumbe wa halmashauri ya kijiji kwa ushirikiani mkubwa waliotoa tangu ujenzi ulipoanza hadi kituo kilivokamilika. “Tunaishukuru Serikali kupitia TASAF (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) kwa kuhakikisha kijiji cha Nyarututu kinasogezewa karibu huduma za Afya kwa Kufadhili Ujenzi wa Zahanati na kuwaepushia adha ya kusafiri kufata huduma mbali. Pia tunawapongeza sana wana kijiji pamoja na uongozi wenu kwa kujitoa na kutoa ushirikiano wa kutosha hadi Zahanati imekamilika”.
Dr Mzee aliwajulisha wajumbe wa kikao kuwa usajili wa Zahanati umekamilika na tayari imeshapatiwa watumishi watatu ambao ni Mganga Mfawidhi na wauguzi wawili, hivyo Zahanati inapaswa kuanza kazi na kuwaomba halmashauri ya kijiji kuhakikisha vifaa vya matumizi ya ofisi vinapatikana kwa nguvu za wana kijiji.Vifaa hivyo ni Mabenchi ya kukalia wagonjwa 10, Meza 8, Viti 16, Kabati la kuhifadhia dawa, maji kwa ajili ya matumizi ya zahanati na kupatika mlinzi wa Zahanati.
Mfamasia wa Wilaya Daniel Mbasagule alisisitiza wajumbe juu ya kutoa elimu sahihi kwa wana kijiji juu ya upatikanaji wa huduma katika zahanati ambazo zinapatikana kwa mifumo mitatu.Mfumo wa kwanza ni wa malipo ya papo kwa papo, mfumo wa matibabu ya bure au msamaha ambayo serikali huchangia kwa wajawazito,watoto chini ya miaka mitano,wazee wa miaka 60 na kuendelea,walemavu na watu wenye magonjwa sugu, na mfumo wa matibabu kwa bima ya jamii ICHF.
Akishukuru kwa niaba ya Kijiji,mwenyekiti wa kijiji Ndg.Felecian Chiza amesema wanaishukuru sana Serikali kwa kuwasogezea huduma ya Afya Karibu ambapo awali iliwalazimu kufata huduma umbali wa Km 5 katika kituo cha Afya Bwanga. Mwenyekiti aliahidi ofisi ya Mganga mkuu kuwa wataendelea kutoa ushirikiano wa karibu muda wote na kuhakikisha vifaa vya matumizi ya ofisi vinapatikana ili kituo kianze kufanya kazi kwa wakati na kwa ufanisi.
Ujenzi wa Zahanati ya Nyarututu ulianza mnamo tarehe 22.01.2025 na kukamilika mwezi Agosti 2025 na kutumia jumla ya Tsh 92,410,714.29 fedha kutoka Serikali kuu (TASAF) na Tsh 7,700,000.00 nguvu za wananchi. Zahanati ilizinduliwa rasmi na Ndg. Ismail Ali Ussi kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa zilizofanyika tarehe 06.09.2025 katika Wilaya ya Chato.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.