Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chato Kaskazini na Chato Kusini Ndg Abel Jonson Manguya, amewakabidhi wagombea wawili Fomu za Uteuzi za kugombea Ubunge ambao ni Ndg Pascal Lucas Lutandula kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akigombea Jimbo la Chato Kusini na Ndg Yohana Costantine Misungwi kupitia Chama cha ACT Wazalendo akigombea Jimbo la Chato Kaskazini.
Tukio hilo limefanyika Agosti 25, 2025 katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Chato Kaskazini na Chato Kusini iliyopo katika jengo la Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi fomu hizo Ndg Manguya amewasihi wagombea wote kuzingatia na kufuata sheria na kanuni za Tume huru ya uchaguzi ikiwa ni6 sambamba na kuhakikisha amani na utulivu vinakuwa sehemu ya mchakato mzima wa uchaguzi huo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki kwani zoezi hilo ni la muhimu kwa Taifa letu.
Aidha Ndg Manguya ametanabaisha kuwa Ofisi yake ipo wazi kwa ajili ya kutoa huduma ya kuwapa wagombea Ubunge fomu za uteuzi kuanzia saa 1.30 Asubuhi hadi saa 10.00 Jioni lakini pia Ofisi za Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata zipo wazi kwa muda huo huo kuhakikisha wanatoa fomu kwa wagombea udiwani.
Zoezi la kutoa Fomu kwa wagombea wa Ubunge na Udiwani lilianza rasmi Agosti 14, 2025 na kutarajiwa kutamatika Agosti 27 huku wagombea wakiaswa kufika kwa wasimamizi wa uchaguzi wakiwa na barua za utambulisho kutoka vyama wanavyoviwakilisha ikiwa ni kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa na INEC , ambapo kauli Mbiu ya Uchaguzi Mkuu kwa mwaka 2025 inasema; "Kura yako ni Haki yako Jitokeza kupiga Kura"
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.