Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mhe. Christian Manunga, jana Januari 28, 2025 aliambatana na timu ya menejimenti ya halmashauri hiyo katika ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi na ukamilishaji wa miradi 7 ya Maendeleo ikiwemo ya Elimu na Afya iliyogharimu kiasi cha shilingi 2,227,125,000/= kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025
Miradi iliyotembelewa ni Ujenzi wa madarasa 2 Mwabasabi Sekondari - Iparamasa (50,000,000/=), Upanuzi wa shule kidato cha 5 na 6 Iparamasa Sekondari (918,125,000/=),Shule Mpya ya Sekondari Mwendakulima - Butengorumasa (584,000,000,/=),Bweni la wasichana Butengorumasa Sekondari (138,000,000/=), Ujenzi wa jengo la OPD zahanati ya Kabantange (92,000,000/=), pamoja na ujenzi wa Sekondari Mpya ya Igogo (114,000,000/=) iliyopo kata ya Buziku.
Mhe. Manunga katika ziara hiyo amesisitiza wasimamizi wa miradi kuzingatia sana nidhamu katika matumizi ya fedha itakayopelekea thamani ya fedha kuonekana kwenye mradi pamoja na kupata majengo yenye ubora ili kutimiza lengo la Serikali kuwa na miundo mbinu imara itakayowawezesha wahitaji kupata huduma kwenye mazingira mazuri na salama lakini pia kuwapunguzia umbali wanafunzi hususani ukamilishwaji wa shule mpya ya Sekondari Mwabasabi na Mwendakulima.
"Binafsi namshukuru sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutujali wana Chato katika suala zima la miundo mbinu hususani ya elimu na afya, ni jukumu letu kumuunga mkono kwa kutumia vizuri fedha anazotupatia kwa ajili ya miradi, wasimamizi wa miradi zingatieni thamani ya fedha (value for money) usimamizi makini wa fedha sambamba na uimara wa majengo bila kusahau huduma bora kwa wananchi tunaowatumikia ndio shukrani pekee tunayopaswa kuipa Serikali yetu ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayofanya" Alisema Manunga
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwabasabi kata ya Iparamasa Mhe. Justiniani Marco Mtunzile, kwa niaba ya wananchi wake amekiri kufurahishwa na Serikali kuwajengea Shule Mpya ya Sekondari Mwabasabi iliyopo kata ya Iparamasa inayotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi wa pili 2025, iliyojengwa kwa lengo la kuwapunguzia wanafunzi umbali wa kilometa 16 kwenda shule ya Sekondari Mnekezi wengi wao wakitokea hapo Mwabasabi.
" Serikali imetujali saana, wanafunzi walikuwa wanakwenda umbali wa kilometa 16 na kurudi tena kilometa 16 kila siku za masomo, lakini kwa sasa watasoma hapahapa Mwabasabi, mimi na wananchi wangu tumekubaliana kuilinda miundo mbinu hii kwa juhudi zote ikiwa ni kuitunza idumu lakini pia kuiunga mkono Serikali yetu sikivu. Alisema Mtunzile
Pamoja na kukagua miradi, pia ziara hiyo ilifanya ufuatiliaji wa kuripoti wanafunzi shuleni mwaka mpya wa masomo 2025 na kubaini kuwa bado kuna wanafunzi wachache hawajaripoti ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Ndg Mandia Kihiyo amewataka watendaji wa kata na vijiji kwa kushirikiana na walimu kuwafuatilia na kuhakikisha wanaripoti shuleni kuendelea na masomo kwani Serikali imefanya kazi kubwa ya kuweka vizuri miundo mbinu na kufanya mazingira ya kujifunzia kuwa salama na rafiki.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.