Na Richard Bagolele-Chato
Mji wa Bwanga uliopo takribani kilometa 50 kutoka mjini Chato na kilometa 60 kutoka mjini Geita unatajwa kuwa ni moja ya maeneo ambayo yapo kimkakati zaidi kukua na kuwa moja ya miji mikubwa hapa wilayani Chato na mkoani Geita kwa ujumla.
Kwa kuliona hilo kuna baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa yaende sambasamba na ukuaji wa mji huo ikiwemo huduma za kijamii na kiuchumi.
Moja wapo ya mambo yaliyomsukuma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Eliurd Mwaiteleke na badhi ya wakuu wa idara kufika katika mji huo na kufanya mkutano mkubwa na wafanyabiashara kwa lengo la kuboresha soko lililopo mjini hapo.
Mkurugenzi alitoa sababu kuu moja na kubwa ya kwanini soko hilo liendelezwe, kwanza ni mahali ulipo mji wa bwanga ni eneo la kimkakati kutoka na kuwa na njia nne kuu zinazoingia na kutoka mjini hapo ikiwemo ile ya barabara inayoelekea Chato Bukoba, Mtukula na Kampala Uganda, Barabara inayoelekea Biharamulo, Ngara, Rusumo hadi Rwanda, njia inayoelekea Runzewe, Kahama, hadi Dar es Salamaam na ile inayoekelea Geita na Mwanza.
Ukiachilia mbali shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya mji huo, Bwanga ina kila sababu ya kuwa mji mkubwa wa kiuchumi hivyo basi kwa pamoja na wafanya biashara wamekubaliana kurekebisha soko hilo hili liweze kuwa la kisasa na la kuvutia watumiaji wengi hususan wanaopita barabara kuu kama nilivyotaja hapo juu.
Mkurugenzi ameenda mbali Zaidi na kusema kuna kila sababu ya wafanya biashara hao kufanya biashara hadi usiku ili kutoa huduma kwa wananchi wanaopita katika eneo hilo kama tu miundombinu itaruhusu ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani katika mji huo ambapo amesema suala hilo linafanyiwa kazi na kabla ya mwaka 2019 kuisha mji huo utakuwa unanga’ra kwelikweli.
Mji wa Bwanga pia hauna kituo cha mabasi hivyo kufanya wananchi wake wapate shida za hapa na pale lakini Mkurugenzi Mtendaji pia amewatoa hofu wafanyabiashara hao kwa kusema kuwa kuna mipango kadhaa ya kujenga kituo kikubwa cha mabasi kitakachokuwa kinahudua wananchi hao.
Mkurugenzi Mtendaji pia alieleza pia kuna kila sababu ya kuupima mji huo ili upangike vizuri na watu waweze kujenga kwa kufuata ramani za mipango miji. Suala hili lilitolewa ufafanuzi mzuri na Mkuu wa Idara ya ardhi na Maliasili Deogratias Matiya ambapo amesema idara hiyo iko kwenyue mpango wa kuhamia hapo kwa ajili ya shughuli za upimaji wa mji huo ili uwe wa kisasa Zaidi.
Eneo la uwekezaji wa viwanda katika mji huu pia ni jambo jingine ambalo Mkurugenzi Mtendaji amesema Halmashauri inalifanyia kazi na kuhakikisha eneo hilo la kimkakati linakuwa na viwanda vya kati na vikubwa ukiachilia mbali shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Kuzinduliwa kwa hifadhi mpya ya Burigi Chato kunaufanya mji huu ukue kwa haraka Zaidi kwa watalii wanaotoka nchi za jirani za Uganda, Rwanda na Burundi, hapa kwa makampuni ya kitalii ni sehemu salama na ya kimkakati kuweka ofisi kwani ni kilometa takrabani 30 kutoka uwanja wa ndege wa Chato lakini mahali hapa utaifikia miji mingine mikubwa iliyopo kanda ya ziwa kama vile Mwanza, Geita, Kahama, Katoro, Buseresere na Bukoba.
Mipango iliyopo hivi sasa ni kuhakikisha mji huo unakuwa na nishati ya umeme ya uhakika ambapo vijiji vyote kwa sasa vina huduma ya umeme kupitia mradi wa REA pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji kutoka ziwa Viktoria.
Naiona Bwanga mpya ile inakuja, bila shaka hii ni mipango kabambe kabisa ya kuubadili mji huu unaokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 33,000 wa maeneo ya Bwanga, Nyakayondwa, Bukirigulu na Izumangabo
Mwandishi wa Makala hii fupi ni Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Wilaya ya Chato 0755773371
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.