Umoja wa kikundi cha ‘Whatsap’ cha Chato Family kimechangia mifuko ya saruji 50 na nondo 12 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa wa sekondari ya Chato.
Akikabidhi vifaa hivyo mmoja ya wanachama wa kundi hilo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro Mhe. Onesmo Buswelu ambaye alihitimu kidato cha nne shuleni hapo mwaka 1996 amesema wameamua kutoa msaada huo ili kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano kwa ujenzi mbalimbali wa miundombinu katika sekta ya elimu ambapo Mheshimiwa Rais Magufuli anajitahidi kuleta maendeleo hivyo ni vyema kumuunga mkono.
“Tunaguswa na kazi za mhe rais... anapambania Taifa hili la Tanzania na Tanzania itajengwa na watanzania wenyewe na sisi kama sehemu ya watanzania ni vyema tuungane nanyi wanachato” alisema Mhe. Buswelu.
Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Chato Mwalimu Selema Bernado amesema Shule hiyo kwa sasa inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa vinane ambapo kwa sasa kuna vyumba vya madarasa 25 tu ukilinganisha idadi kubwa ya wanafunzi 1520 waliopo shuleni hapo.
Mwalimu Bernado pia amesema shule hiyo inakabiliwa na Chumba cha Maabara ya Sayansi, ofisi za walimu ambapo husababisha baadhi ya vyumba vya madarasa kutumika kama ofisi ya walimu. Amewashukuru wanakikundi hao kwa msaada huo na kuomba wadau wengine wajitokeze katika kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi shuleni hapo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji afisa elimu taaluma wa Sekondari Masai Mjule amewashukuru wanakikundi hao kwa mchango wa vifaa hivyo na kusema kuwa upatikanaji wa mchango huo kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.
Chato Family ni kundi la ‘whatsap’ linaloundwa na baadhi wanafunzi waliowahi kusoma sekondari ya Chato na watumishi waliowahi kufanya kazi Wilayani hapa.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.