Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chato Ndg. Mandia H. Kihiyo Januari 20/2024 ameendelea na ziara yake ya kata kwa kata shule kwa shule, kutembelea shule zote za Sekondari lengo likiwa ni kufuatilia wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopangwa na walioripoti shuleni.
Katika ziara hiyo Ndugu Kihiyo alikutana na timu ya uongozi kuanzia ngazi ya kijiji, Kata, walimu pamoja na wanafunzi ndipo aliwataka kila mmoja atimize majukumu yake kwa uweledi lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni na walimu kusimamia ufundishaji wenye tija kwa kuzingatia ratiba ya vipindi kwa kadri miongozo inavyowaongoza ili kukuza viwango vya ufaulu.
Aidha aliwataka viongozi hao kuendelea kuwa mfano mzuri katika suala la nidhamu pamoja na kusimamia maadili ya wanafunzi na kuhakikisha wanawalinda dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kuwapata wakiwa mazingira ya shuleni lakini pia katika mazingira ya makazi yao.
Ziara ya Mkurugenzi ilianza mara tu shule zilipofunguliwa Januari 8/2024 ambapo pamoja na kufuatilia wanafunzi walioripoti na wasioripoti pia amewataka watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanafunzi wote ambao bado hawajaripoti shuleni kufikia Januari 20/2024 wawe wameripoti.
"Jukumu letu viongozi ni kufanya kazi kwa ufanisi, Serikali imejenga miundo mbinu mizuri sana katika shule sasa wanafunzi wasipokuwepo itafaa nini? Viongozi wa vijiji na kata wafuatilieni wale wote waliokaa na wanafunzi nyumbani hakikisheni wanaripoti kufikia Januari 20, Pia suala la chakula shuleni lazima lipewe umuhimu mkubwa na mikakati ya kuinua ufaulu iwekwe na kuzingatiwa ili kufanikiwa haya yote hakikisheni nidhamu inapewa kipaombele kwa kila mmoja" Alisema Kihiyo.
Mpaka kufikia Januari 19/2024 tayari alikuwa ametembelea robo tatu ya shule zote zilizopo wilaya ya Chato imebainika kuwa ufuatiliaji huu wa shule kwa shule umezaa matunda kwa kiasi kikubwa kwani taarifa zimekuwa zikiwafikia wazazi waliokaa na wanafunzi nyumbani na kupelekea wimbi la kuripoti wanafunzi kuongezeka hivyo lengo la ziara kutimia.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.