Mkuu wa Wilaya ya Chato Martha Mkupasi ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya hiyo na maeneo jirani na mkoa wa Geita kwenda kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Kanda iliyopo wilayani hapo kwani kwa sasa hospitali hiyoinavifaa vya kutosha na inatoa huduma za kibingwa kwa magonjwa yote.
Wito huo umetolewa leo kwenye ufunguzi wa juma la maadhimisho mwaka mmoja wa utoaji huduma ya Hospitali hiyo ambayo ilianza kutoa huduma za rufaa tarehe 30 Julai 2021.
Mkuu wa Wilaya amesema kwa sasa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imepokea vifaa vingi hivyo ni vyema jamii ikaelewa kuwa hospitali hiyo ipo tayari kupokea wagonjwa wa aina yoyote kutoka maeneo ya karibu na mkoa wa Geita .
“Kwa sasa hospitali ina wataalamu wengi waliobobea, ina vifaa vingi na vizuri leo tumejionea wenyewe ndani ya hospitali hii, ni Imani yangu wagonjwa watatibiwa vizuri na kwa wakati” amesema Mkuu wa Wilaya ya Chato.
Mbunge wa jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani ameishukuru serikali ya awamu ya sita kuendelea kutoa fedha kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ambapo amesema kukamilika kwa hospitali hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imesaidia wananchi wa Chato na mkoa wa Geita kwa ujumla kupatiwa matibabu kwa gharama nafuu na haraka kwani hapo awali walilazimika kwenda Mwanza kwa ajili ya matibabu.
“Mheshimiwa Rais atembee kifua mbele, fedha anazoleta tunaona zinafanya kazi nzuri, na sisi tunamhakikishia tutalinda miundombinu ya hospitali hii kwani matunda yake tunayaona” amesema Mhe. Dkt. Medard Kalemani
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Dkt. Oswald Lyapa amesema hospitali hiyo imeweza kuhudumia wagonjwa 10,502 tangu ianze kutoa huduma tarehe 30 Julai 2021. Amesema wagonjwa wengi wanaopatiwa huduma wanatoka mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma na Shinyanga.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato ilianza kujengwa mwaka 2017 na inakadiriwa kutoa huduma kwa wagonjwa 700 hadi 1000 kwa siku. Kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma za kibingwa za upasuaji, huduma za mama na mtoto, magonjwa ya ndani, huduma za utoaji dawa na vifaa tiba, huduma za uchunguzi wa afya na huduma za mionzi.
Hadi sasa ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 25 ambapo kwa sasa serikali kupitia fedha za UVIKO 19 imetenga shilingi bilioni 6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ikiwa ni pamoja na CT Scan, MRI,X-Ray pamoja na vifaa vya wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharula.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.