Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Wilaya ya Chato imeziagiza taasisi zote za Serikali Wilayani hapa kuhakikisha miradi yote inayo anzishwa inakamikika kwa wakati na kwa ubora ili iweze kuwa na manufaa kwa jamii.
Agizo hilo limetolewa na wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Chato walipofanya ziara ya siku moja yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri pamoja taasisi za serikali Serikali zilizopo Wilayani hapa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chato ndugu Raphael Masambo amesema pamoja na Wilaya ya Chato kuwa na miradi mingi mizuri lakini miradi hiyo imekuwa haikamiliki kwa wakati hivyo kusababisha usumbufu kwa jamii pamoja na kusuasua kwa utekelezaji wa ilani ya CCM.
"Niwaombe sana kamilisheni hii miradi haraka itoe manufaa kwa wananchi" alisema ndugu Raphael Masambo wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Nyarutembo.
Mbunge wa jimbo la Chato Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanasimamia vizuri matengenezo ya Barabara ya Bwera hadi Busaka inayokarabatiwa na kampuni ya Clearing ya Mwanza ambapo imefanyiwa matengenezo lakini si ya kiwango cha kuridhisha.
"TARURA hakikisheni mnasimamia hizi barabara ziweze kudumu na thamani ya fedha ionekane" alisisitiza Mhe. Kalemani.
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi ameonya tabia ya baadhi ya wakandarasi wa miradi ya maji kutokuwepo kwenye maeneo ya miradi kitendo ambacho kinafanya miradi mingi kutokukamilika kwa wakati na kusababisha usumbufu kwa wananchi kukosa huduma za mhimu.
Amwemwagiza mkandarasi anajenga mradi wa maji kijiji cha Busaka TANAFR wa Kigoma kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati vinginevyo ataagiza RUWASA ivunje mkataba na Mkandarasi huyo.
Wajumbe hao pia wamemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha fedha zinazopelekwa kwenye miradi ya maendeleo hususan ule wa ujenzi wa Zahanati ya Mabila kata ya Makurugusi unafanyiwa uhakiki wa matumizi ya fedha kiasi cha shilingi milioni 50 zilizopelekwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo.
Kamati hiyo pia imemwagiza mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha anasimamia ukamilishaji wa ujenzi wa kituo cha Afya Nyarutembo, kituo cha Afya Nyabilezi na kukamilisha ujenzi wa kituo cha Mabasi cha Kahumo ifikapo tarehe 30 Septemba 2022.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.