Maafisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato wamepatiwa maelekezo maalumu kuhusu utekelezaji wa kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya homa ya mapafu ya ng'ombe itakayoambatana na zoezi la uvalishaji wa hereni za utambuzi wa Mifugo hiyo.
Maelekezo hayo maalumu walipatiwa Agosti 25, 2025 katika ukumbi mdogo wa mikutano uliopo halmashauri Ofisi za Uthibiti ubora wa Shule huku mgeni rasmi akiwa ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg Geriad Mgoba ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (W).
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Ndg. Mgoba aliwataka wataalamu hao kuzingatia maelekezo waliyopewa pamoja na kutumia vizuri taaluma yao wakati ukifika wa utekelezaji wa chanjo hiyo inayotarajiwa kuanza mnamo Septemba 01, 2025, na kuzinduliwa rasmi katika kata ya Nyamirembe, huku Mgeni rasmi wakati wa ufunguzi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Louis Peter Bura.
Mgoba ameeleza kuwa halmashauri hiyo tayari imeshapokea Chanjo kwa ajili ya homa ya mapafu kwa ng'ombe (CBPP), vifaa vya kuchanjia pamoja na vitendea kazi vya kuendesha zoezi hilo kwa wilaya nzima.
Naye Daktari wa wanyama (DVO) Chato, Dkt. Sosthenes J. Nkombe alisema wataalamu hao wamepata maelekezo na wapo tayari kuanza zoezi hilo, ambapo alifafanua kuwa wanatarajia kuchanja, kuweka hereni za utambuzi na kusajiri jumla ya Ng'ombe 111,659 waliopo wilayani humo, alieleza madhara yanayoweza kutokea endapo mifugo hiyo haitachanjwa kuwa ni pamoja na vifo vya mifugo hiyo vitakavyopelekea hasara kwa wafugaji hivyo ni zoezi muhimu kwa manufaa ya Taifa.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.