Jumla ya wananchi 21,693 wa kata ya Bwongera wilayani Chato wanatarajia kunufaika na kituo kipya cha Afya cha kata hiyo kinachojengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ambapo kinatarajiwa kugharimu shilingi milioni 500 pamoja na nguvu za wananchi.
Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashari ya Wilaya ya Chato ndugu Mandia Kihiyo wakati wa ziara ya kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ya Halmashuri ikikagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri kupitia mapato ya ndani ilitenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha hicho cha afya ikiwa ni sehemu ya fedha za asilimia 40 ya mapato ya ndani zinazotengwa kila mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
"Hadi sasa tumekwishaleta hapa shilingi milioni 201 na lengo letu ni kukamilisha kituo hiki mwezi Septemba mwaka huu ambapo kwa mwaka huu tutajenga kituo kingine cha Afya Kata ya Ichwankima" alisema Mkurugenzi Mtendaji.
Mbunge wa Jimbo la Chato Mhe. Dkt. Medard Kalemani amepongeza baraza la Madiwani la Halmashauri kwa uamuzi wa kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kituo hicho ambapo amesema ujenzi wa kituo hicho ni maamuzi mazuri na ya kupongezwa ameomba kamati hiyo kuhakikisha kituo hicho kinakamilika kwa wakati ili kianze kutoa huduma.
"Nikupongeze Mkurugenzi na timu yako ya wataalamu, mnafanya kazi nzuri sana, nimefanya kazi na wakurugenzi wengi lakini huyu anafanya kazi nzuri anastahili pongezi tusimkatishe tamaa" alisema Dkt. Kalemani
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mhe. Christian Manunga ambaye pia ni diwani wa Kata ya Bwongera amesema kukamilika kwa kituo hicho kutanufaisha wakinamama wengi wa kata hiyo ambao wamekuwa wakipata ugumu wakati wa kujifungua ambapo wamekuwa wakipata huduma katika zahanati ndogo iliyopo katika eneo hilo na wengine wamekuwa wakihudumiwa kwenye kituo cha Afya cha Muganza ambapo ni mbali kutoka eneo hilo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Dkt. David Mndeba amesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia wananchi wengi wakiwemo wa kata hiyo pamoja na Wilaya jirani ya Muleba ambao wamekuwa wakifika katika zahanati ya kijiji hicho.
Kituo cha Afya cha Katete kilianza kujengwa mwezi Desemba 2021 ambapo kuna jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la upasuaji na wodi ya wazazi ambapo jumla ya shilingi milioni 500 za mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na nguvu za wananchi zinatarajiwa kukamilisha kituo hicho mnano mwezi Septemba 2022.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.