Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Said Nkumba amewataka maafisa taaluma, Tume ya utumishi wa walimu (TSC) pamoja na wathibiti ubora wa shule wilaya, kusimamia kikamilifu masuala ya taaluma shuleni ili kuongeza kasi ya ufundishaji itakayoinua wastani wa ufaulu katika wilaya hiyo.
Nkumba alitoa maelekezo hayo katika kikao kazi cha elimu kilichofanyika April 09, 2024 katika ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana Jikomboe kilichojumuisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, wakuu wa idara na vitengo, maafisa elimu kata, wakuu wa shule, walimu wakuu pamoja na wadau wa elimu
" Tuweke mikakati mizuri na kuisimamia ili kuinua ufaulu katika wilaya yetu hususani kudhibiti utoro na nidhamu kwa wanafunzi, kuwapa chakula wanafunzi wote bila kubagua, kuwapa motisha walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri, wakuu wa shule kusimamia nidhamu ya walimu walioko chini yao ikiwa ni pamoja na mahudhurio na mavazi yao kazini huku wakihakikisha walimu wanajindaa kabla ya kuingia darasani kufundisha. " Alisema Mhe Nkumba.
Pia alisisitiza mahusiano mazuri kazini ili kuleta ufanisi wa kazi hatimaye matokeo chanya ambapo aliwataka walimu wakuu na wakuu wa shule kuimarisha mahusiano yao na viongozi wa kata na vijiji ili kufanya kazi kama timu kuwafuatilia wanafunzi watoro na kidato cha kwanza wasioripoti shuleni, huku akipongeza uandikishwaji wanafunzi wa darasa la awali kuvuka lengo kwani maoteo yalikuwa ni 19,646 na walioandikishwa ni 24,306 kwa mwaka 2024 sawa na 124.8/%
Akitoa taarifa ya idara kwa niaba ya Afisa elimu shule za msingi Bi Rehema Mkalola ambaye ni Afisa elimu elimu ya watu wazima msingi alisema Chato ina jumla ya shule za awali na msingi 168 ambapo kati ya hizo za Serikali ni 154 na 14 ni za watu binafsi na mashirika ya dini, shule za Serikali zina jumla ya wanafunzi 159,121 kati yao ME 78,632 na KE 80,489 huku shule za binafsi na mashirika ya dini zikiwa na jumla ya wanafunzi 2,507 kati yao ME 1,273 na KE 1,234 ikiwa jumla ya walimu ni 1,967 kati yao ME 1,266 na KE 701.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.