Mkuu wa Wilaya ya Chato Shaaban Ntarambe ameendelea kuonya tabia ya baadhi ya wananchi wa Wilaya hiyo ya kuendekeza ulevi nyakati za asubuhi na mchana badala ya kufanya kazi.
Mkuu wa Wilaya ametoa onyo hilo leo wakati alipofanya mkutano wa hadhara na wananchi wa tarafa ya Nyamirembe mkutano uliofanyika mjini Muganza.
“Mikutano hii nawahimimiza watu wafanye kazi… wapo watu wanafanya kazi kwa kubetuabetua na kazi yao ni kunywa pombe tu, ieleweke mida ya kunywa pombe tena ile halali ni kuanzia saa 9.30 alasiri hadi saa 1 jioni na si asubuhi au mida ya kazi, tena pombe ziuzwe kwenye maeneo maalumu tu sio kila nyumba na mkinywa msilewe” alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya amewahimiza wananchi wa tarafa ya Nyamirembe kuendelea kuchangia ujenzi wa miuondombinu ya sekta za elimu na afya ili kufikia lengo ambalo serikali ya mkoa wa Geita umejiwekea la kuwa na zahanati katika kila kijiji pamoja na uwepo wa vyumba vya madarasa vya kutosha kwenye shule za msingi na sekondari.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Chato ametoa agizo kwa wazazi na walezi ambao hawajapeleka watoto wao kuandikishwa kuanza elimu ya msingi kuhakikisha wanawapeleka mara tu shule zitakapofunguliwa mapema mwezi Julai. Amezitaka serikali za vijiji kuchukua hatua mara moja kwa wazazi au walezi watakao kaidi agizo hilo. Mkuu wa Wilaya amesema kuwa kila mzazi au mlezi anao wajibu wa kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule hata kama hawana sare za shule.
Mkuu wa Wilaya pia amewataka wananchi kuwaondoa viongozi wa serikali za vijiji ambao hawaitishi mikutano halali ya kisheria kwa vijiji husika endapo hawataitisha mikutano mitatu mfulilizo kama sheria za mikutano zinavyoeleza.
Mkuu wa Wilaya yuko kwenye ziara ya kuongea na wananchi wa tarafa zote tano za Chato ili kuhimiza wananchi kufanya kazi, kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja, kutoa ufafanuzi mbalimbali wa masuala ya kiserikali pamoja na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.