Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amewataka viongozi wa Mkoa wa Geita kusimamia vyema fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali ili ziweze kuleta tija katika jamii.
Ndugu Chongolo ametoa maagizo hayo leo Novemba 16, 2021 Wilayani Chato Mkoani Geita wakati akipokea taarifa ya Mkoa ya Chama Cha Mapinduzi kwenye ukumbi wa CCM wilaya ya Chato.
Amesema serikali kwa nyakati fofauti imekuwa ikitoa fedha kwenye miradi mbalimbali kwa lengo la kuleta matokeo yanayotarajiwa lakini fedha hizo zimekuwa hazitatui matatizo ya jamii husika.
Ndugu Chongolo amesema serikali imetoa fedha shilingi bilioni 17 kwa mkoa wa Geita ili ziweze kusaidia katika ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari hivyo amewaagiza viongozi hao kusimamia fedha hizo kwa umakini.
Ameupongeza uongozi wa mkoa wa Geita kwa kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje kupitia hospitali ya rufaa ya kanda iliyopo Chato ambapo amesema hospitali hiyo itasaidia mikoa ya kanda ya ziwa.
Ndugu Chongolo pia amezitaka Halmashauri kutoa asilimia 10 za fedha ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa wakati ili zisaidie mitaji ya vijana, wanawake na walemavu, "tuache kuzikumbatia, tuache kuzitoa kama zawadi, tuzitoe kwa sababu ni utaratibu na zirejeshwe kwa utaratibu" amesisitiza ndugu Chongolo
Aidha Katibu mkuu wa CCM amewaasa viongozi wa Mkoa wa Geita kufanya kazi kwa upendo na ushirikiano na kwa kuheshimiana kila mmoja kwa kutokuangalia nafasi walizonazo viongozi bali waangalie ubora wa chama.
Imetolewa na Richard Bagolele-Chato
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.