Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Louis Bura akiwa ameambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama pamoja na timu ya wataalam ngazi ya wilaya wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo Dkt. Aristides Raphael, wametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya wilaya hiyo.
Ziara hiyo imefanyika leo Disemba 18, 2024 ambapo miradi 11 imetembelewa na kukaguliwa, huku miradi mingi kati ya hiyo ikionekana kuridhisha na mingine kuibuka kidedea kwa ukamilishwaji wa haraka, viwango vya ubora pamoja na thamani ya fedha kuonekana huku chenji ikibaki hususani mradi wa Bwalo la chakula Makurugusi Sekondari pamoja na Zahanati ya kijiji cha Butengorumasa.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni Ujenzi wa bwalo la chakula Makurugusi Sekondari (175,000,000/=), Shule mpya ya Igogo Sekondari - Buziku (114,400,000/=), Nyumba ya watumishi 2 in 1, Mabweni 2 na vyoo matundu 12 Kabantange Sekondari (381,000,000/=), Jengo la X-rays Kituo cha afya Bwanga (58,468,176/=), Shule mpya ya Sekondari Mwendakulima (584,000,000/=), Shule Mpya ya kidato cha 5&6 Iparamasa (853,725,000/=), Ujenzi wa Daraja la Muranda - Imwelu (400,000,000/=), pamoja na ukaguzi wa utoaji huduma kituo cha afya Mapinduzi na kituo cha afya Iparamasa.
Mhe. Bura amewapongeza wasimamizi wa miradi hiyo kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kwa umakini, kuhakikisha wanazingatia vigezo vya ubora wa majengo unaohitajika na Serikali huku akiwaasa wachache wenye changamoto katika ukamilishaji wa miradi kuhakikisha wanarekebisha tofauti zilizojitokeza na kuwataka wajifunze kwa waliofanikiwa.
"Ninawapongeza sana wasimamizi kwa jinsi mnavyotekeleza miradi hii kwa ubora na thamani ya fedha inaonekana, lakini Shukrani nyingi zaidi ni kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa kutuletea fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo wilayani Chato, ni jukumu letu kuhakikisha tunasimamia vizuri ili kupata majengo yenye ubora na hatimaye nia ya Serikali yetu itimie watoto wetu waweze kukuta miundo mbinu imekamilika shule zitakapofunguliwa Januari 2025 lakini kwa upande wa afya tukamilishe ili huduma zianze kutolewa mapema kuwapunguzia umbali wananchi." Alisema Mhe. Bura.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Butengorumasa Mhe. Makoye Daud Cosmas amekiri kufurahishwa na ukamilishwaji wa mradi wa zahanati ya kijiji hicho kwa wakati na kwa kubakiza chenji kwani ilijengwa kwa nguvu za wananchi kwa Tsh. 19,521,000/=, na kisha wakala wa misitu (TFS) kuwapatia kiasi cha Tsh 100,000,000/= ambayo walitumia 85,162,900/=kukamilisha zahanati hiyo na kusalia Tsh. 14,837,100/= fedha ambayo wataifanyia shughuli nyingine za maendeleo.
" Ninaupongeza uongozi wote wa wilaya ya Chato kwa kuuweka mbele uzalendo katika kutekeleza miradi ya maendeleo, usimamizi madhubuti wa miradi kuanzia kwa Mhe. DC, Mkurugenzi, wataalam ngazi ya wilaya, Kata, pamoja na wasimamizi ngazi ya kijiji ndio chanzo cha mavuno bora ya miradi yetu hapa wilayani Chato, Serikali yetu ya awamu ya sita inafanya kazi kwa vitendo kila mmoja anapaswa kuiunga mkono kwa uaminifu na utii." Alisema. Cosmas
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.