Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) imefika wilayani Chato mkoani Geita kwa lengo la kujiridhisha iwapo vigezo vilivyowekwa na Tume hiyo katika majimbo yanayoomba kugawanywa vimezingatiwa ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi.
Aidha ziara hiyo siyo kigezo cha moja kwa moja kuwa Jimbo limegawanywa badala yake jamii inapaswa kutambua kuwa hatua hiyo ni matakwa ya kanuni za Tume huru ya taifa ya Uchaguzi zinazoelekeza kufika katika majimbo husika kukagua na kupokea maoni ya wadau.
Akizungumza na wadau mbalimbali katika kikao maalumu kilicholenga kukutana na wadau pamoja na kupokea maoni yao,Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) ambaye pia ni Jaji wa mahakama kuu, Asina Omari, amesema Tume hiyo inaendelea na mchakato wa kukagua vigezo mbalimbali katika majimbo yaliyoomba kugawanywa.
Kwa mujibu wa Jaji Asina,Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 75(4) na 74(6)(c) ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi namba 1 ya mwaka 2024,Tume inajukumu la kuchunguza na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya Uchaguzi.
"Aidha Tume inaweza kutekeleza jukumu ilo mara kwa mara au angalau kila baada ya miaka 10,"
"Ibara ya 75(3) na (4) imeainisha vigezo vya ugawaji wa majimbo ambayo ni idadi ya watu,upatikanaji wa mawasiliano,na hali ya kijiografia,vigezo vingine vinavyozingatiwa na Tume katika kugawa majimbo vimeainishwa katika jedwali la tatu la kanuni za Tume huru ya Uchaguzi za mwaka 2024" amesema Jaji Asina.
Kadhalika Jaji Asina, amesema vigezo vingine ni hali ya kiuchumi,ukubwa wa eneo la Jimbo husika,mipaka ya kiutawala, Jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi, Mazingira ya Muungano na uwezo wa ukumbi wa Bunge.
Baadhi ya wadau waliohudhuria kikao hicho,akiwemo Diwani wa Chato,Mange Ludomya na Diwani wa kata ya Minkoto,George Magezi, wameihakikishia INEC kuwa taarifa zote zilizoainishwa kwenye maombi ya kuligawanya Jimbo la Chato yalizingatia taratibu na kanuni zote ikiwa ni pamoja na vikao halali vya maamuzi.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.