Wakazi wa Kijiji cha Kinsabe kata ya Iparamasa wilayani Chato mkoani Geita wameipongeza mamlaka ya usambazaji maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) baada ya kuwanusuru na adha ya kutumia maji ya madimbwi kwa kishirikiana na fisi.
Aidha kijiji hicho hakijawahi kupata maji ya bomba tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika(Tanzania bara) na kwamba kitendawili hicho hatimaye kimeteguliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Pongezi hizo zimetolewa na Chausiku Bomba(65) mkazi wa kijiji hicho ambaye pamoja na mambo mengine amesema kabla ya Mradi huo walikuwa wakitumia maji machafu huku wakichangia na wanyama wa kufugwa na wale wa polini hali iliyokuwa ikiwasababishia kuugua magonjwa ya matumbo mara kwa mara.
Khadija Khamis, amesema upatikanaji wa maji hayo umesaidia baadhi ya wananchi kuvuta maji ya bomba kwenye makazi yao na kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kijiji jirani kutafuta huduma hiyo jambo lililo saidia kupatikana utulivu wa familia ukilinganisha na awali kabla ya kupatikana huduma ya maji ya bomba.
"Sasa hivi kwa kweli angalau tuna amani katika familia zetu,maana awali watoto wetu walikuwa wanatoka shule na kwenda kutafuta maji, lakini huko njiani wanakutana na vishawishi vya kila aina na wakati mwingine wanatishwa na fisi na kulazimika kurejea nyumbani bila maji" amesema Khadija.
Akielezea utekelezaji wa mradi huo mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Meneja wa usambazaji wa maji na Usafi wa Mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Chato, Mhandisi Avitus Exavery, amesema mradi huo wa Kinsabe umekamilika kwa aslimia 98 na kwamba kaya 16 zimevuta maji majumbani huku zaidi ya wakazi 7,040 wanatarajia kunufaika kwa kutumia maji safi na salama.
Amesema mradi huo wa kisima kirefu chenye urefu wa mita 72 una uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 12,000 kwa siku na kwamba umetekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 335.2 kwa lengo la kuondoa changamoto za upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kijiji cha Kinsabe na vitongoji vya Beda,Kinsabe,Elimu, Nyangugunwa A na Nyangugunwa B.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.