Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Louis Peter Bura jana Mei 12, 2025, aliambatana na timu yake pamoja na wataalamu kutoka halmashauri alifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya Maendeleo inayotekelezwa wilayani hapo itakayogharimu kiasi cha Tshs. 1,033,997,446/=.
Akizungumza na wananchi wakati wa ukaguzi wa miradi Mhe. Bura ameipongeza na kuishukuru sana Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayofanya kuleta fedha za kujenga na kuboresha miundombinu kwa kila sekta, jukumu kubwa tulilo nalo ni kuilinda na kuitunza jambo ambalo litahamasisha kuletewa miradi mingine.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kanyindo (71,642,655/=) zahanati ya kijiji cha Nyarututu (92,410,714/= TASAF), Bweni la wasichana shule ya Sekondari Butengorumasa (138,264,042/= TASAF), Shule mpya ya Sekondari Ihanga (114,400,000/= ), Shule mpya ya Sekondari Mwendakulima (584,280,029/=), Bweni la wasichana shule ya Sekondari Mkungo (138,264,048/= TASAF) Pamoja na kukagua utoaji wa huduma kituo cha afya Malebe ambacho tayari kimepokea kiasi cha 33,000,000/= kwa ajili ya kichomea taka, shimo la majivu, shimo la kutupa kondo na mnara wa tenki la kuweka maji na kuyasambaza.
Aidha Mhe. Bura alipongeza kamati pamoja na wasimamizi wa asilimia kubwa ya miradi aliyoikagua, kutokana na ubora wa kiwango kizuri kinachotakiwa na Serikali, hali inayodhihirisha kuwa usimamizi wa fedha za umma ulikuwa ni mzuri, hatimaye umeleta matokeo chanya yanayotarajiwa na wananchi, huku akisisitiza jambo la uaminifu katika suala zima la usimamizi wa miradi kuwa endelevu na lipewe uzito ili kupata miradi bora inayoendana na thamani ya fedha.
'Ndugu zangu maendeleo haya tunayoyaona ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo nimetembelea na kukagua miradi ya zaidi ya Tsh. Bilioni moja fedha ambazo zimeletwa kwa ajili yetu wana Chato, kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali hususani elimu na afya, mama hana deni kabisa kwetu, bali sisi tuna deni kubwa sana la kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iwe chachu ya kutuletewa mingine. Alisema Mhe. Bura.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.