Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato ndugu Mandia Kihiyo amewataka watumishi walio katika sekta ya elimu wilayani hapa kujitathimini kwa matokeo mazuri ya ufaulu wa wanafunzi kwa ngazi ya Wilaya hadi taifa.
Mkurugenzi Mtendaji ameyasema hayo leo jumatatu tarehe 13.12.2021 wakati akifungua mafunzo kwa maafisa elimu kata na walimu wakuu yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu kupitia idara ya uthibiti ubora wa shule Wilaya ya Chato yaliyofanyika sekondari ya Chato.
Mkurugenzi Mtendaji amesema pamoja na Wilaya ya Chato kufikia malengo ya ufaulu, bado kuna jitihada zinatakiwa zifanyike ili kuendelea kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na cha sita.
"kupitia mazuri ya kikao kikao hiki na kwa matokeo tutakayopata yatusaidie kujua tumefanya nini, tathmini hiyo itusaidie kujipima na tuweze kupanga mipango mizuri kwa mwaka ujao ambapo lengo letu ni kufikia ufaulu wa asilimia 90 kama tulivyokubaliana chini ya timu hii" amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa upande wake Mkuu wa idara elimu msingi Wilaya ya Chato ndugu Omari Mkombole amesema Wilaya ya chato inaendelea kufanya vizuri kwenye ufaulu wa mitihani ya darasa na nne na la saba hivyo ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili walimu ikiwemo malipo ya nauli na likizo ili ziwafikie kwa wakati huko walipo kutokana na timu aliyounda kushughulikia madai hayo.
Aidha ndugu Mkombole amepiga marufuku tabia ya walimu kutoka kwenye vituo vya kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa barua kwenye ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na badala yake ameagiza barua zote ziratibiwe na ofisi ya afisa elimu kata na kisha kufikishwa kwa pamoja ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji,
"mimi kwenye idara nimesema kwamba barua ya mwalimu itapitia kwa malimu mkuu, itaenda kwa afisa elimu kata naye atafanya jitihada za kuja yeye mwenyewe au atatuma mwalimu mmoja alete pamoja na sisi tutashughulikia haraka na si kama inavyofanyika sasa hivi ambapo kila mwalimu anafuatilia yeye mwenye" alisema ndugu Mkombole.
Mthibiti mkuu wa ubora wa shule Wilaya ndugu Justina Grassiano amesema baada ya mafunzo hayo walimu wakuu wote katika Wilaya ya Chato watakuwa wameimarishwa katika suala zima la uthibiti ubora wa ndani, ambapo wanatarajia mafunzo hayo yatasaidia kupata tathimini ya ufundishaji na ujifunzaji na hivyo Wilaya itakuwa katika nafasi ya kufanya mabadiliko chanya kwa wakati kulingana na matokeo ya tathimini ya ndani.
Mafunzo hayo yameshirikisha maafisa elimu kata 20 na walimu wakuu 99.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.