Msimamizi wa Uchaguzi Mkuu Jimbo la Chato Kusini na Chato Kaskazini Ndg. Abel Johnson Manguya leo Agosti 4, 2025 amezindua rasmi mafunzo maalumu kwa wasimamizi wasaidizi 46 wa uchaguzi ngazi ya kata, kutoka kata 23 ambayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia tar 04 - 06, 2025 katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya ufundi Chato.
Akifungua mafunzo hayo Ndg Manguya amewapongeza wasimamizi hao kwa kuaminiwa na kuteuliwa huku akiwataka kuzingatia mafunzo wanayopewa ili wakatekeleze majukumu yao kikamilifu kwa uadilifu, kufuata sheria, kanuni, na taratibu za Uchaguzi Mkuu ili kufanikisha jambo hili nyeti lenye manufaa makubwa kwa Taifa.
"Kazi ya usimamizi wa uchaguzi ni jukumu nyeti linalohitaji umakini na uaminifu mkubwa, pamoja na mafunzo haya pia msome na kuelewa vizuri katiba, sheria, kanuni taratibu, miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kushirikisha vyama vyote vya Siasa vyenye usajili kamili kwa mujibu wa Sheria, epuka kuwa chanzo cha malalamiko katika suala zima la utekelezaji wa majukumu yako ili zoezi hili muhimu likamilike kwa ufanisi. Alisema Manguya"
Mafunzo hayo yameanza mara baada ya wasimamizi hao ngazi ya kata kuapishwa rasmi na Mhe. Tryphone A. Bashaya, Hakimu Mkazi Mfawidhi, kwa lengo la kuimarisha uaminifu katika zoezi zima la uchaguzi lakini pia kuonesha utii wa sheria huku wakikiri kufanya kazi hiyo nyeti kwa weledi na uaminifu mkubwa.
Naye Mwenyekiti wa Mafunzo Ndg Mussa Nyanda ambaye ni miongoni mwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata amesema mafunzo hayo yatawapa uelewa wa pamoja na kuwajengea uwezo mzuri wa kutekeleza majukumu kwa kufuata miongozo na maelekezo waliyopewa hatimaye kukamilisha zoezi la uchaguzi Mkuu kwa amani.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa shughuli nzima ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge, na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, huku kauli Mbiu ikisema:
"Kura yako Haki yako Jitokeze kupiga Kura"
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.